NIPASHE
Ukitaka kuona sura halisi za wabunge wa Tanzania gusa posho zao, huo ndio  msimamo wao wa miaka na miaka na jana ulijidhihirisha kufuatia ushauri wa Waziri  Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, wa kutaka kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge  katika bajeti ya serikali ya mwaka 2011/2012.
 Jana baadhi ya wabunge hasa wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM), walipinga kwa nguvu zao zote mapendekezo ya Zitto ya kutaka posho za  vikao wanazolipwa ziondolewe.
 Wa kwanza kupinga mapendekezo hayo bila hata  kutafuna maneno alikuwa ni Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), John Chiligati,  ambaye alisema kama wabunge wa kambi ya upinzani hawataki kuzipokea fedha hizo  waziache.
 Chiligati alitoa msimamo huo jana jijini Dar es  Salaam, alipotakiwa kutoa maoni yake kama anaona kuna haja posho za wabunge  kuondolewa kama ilivyopendekezwa na Naibu kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni,  Zitto Kabwe.
 Akizungumza na NIPASHE katika viwanja vya ofisi za  Bunge jijini Dar es Salaam, Chiligati ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM  (Bara), alisema hoja hiyo sio ya wabunge wote bali ya upinzani na hivyo kama wao  wanaona hawazihitaji posho hizo wasizichukue.
 “Hii kambi ya upinzani kama haitaki hailazimishwi  kupokea posho hizo za vikao wanaweza kuziacha sio lazima wazipokee,”  alisema.
 Naye Mbunge wa Magomeni visiwani Zanzibar,  Mohammad Chomboh (CCM), alisema suala hilo halitekeleziki kwa kuwa Sh. 80,000  anayolipwa mbunge kama posho ni ndogo ikilinganishwa na hali halisi ya maisha  ilivyo sasa.
 Alisema kulala nyumba ya wageni kwa siku  wanapokuwa Dodoma ni Sh. 50,000 hapo bado hawajala hivyo kiasi hicho sio kikubwa  kama inavyoelezwa na upinzani.
 Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza (CCM),  alisema hoja ya kutaka posho ifutwe ni mawazo ya mtu kwani waliopanga malipo ya  posho hiyo nao pia wana sababu zao.
 Hata hivyo, alimtaka mbunge yeyote mwenye hoja  kama hiyo, aipeleke bungeni ikajadiliwe huko, badala ya kuizungumzia nje ya  Bunge.
 Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamisi Kigwangalla,  alisema haungi mkono hoja ya Zitto, kwa vile imejaa unafiki na kujitafutia  umaarufu.
 “Kama kweli tuna dhamira ya msingi ya kutumikia  Watanzania kuna vitu vingi vilipaswa viondolewe na si posho peke yake. Kwa  mfano, mashangingi yangefutwa kwa sababu yana gharama kubwa kuendesha.
 Lakini yanahitajika kwa wabunge kutumia kuwafikia  wananchi vijijini,” alisema Dk. Kigwangalla.
 Alisema posho za vikao, ambazo Zitto anataka  zifutwe, ni ndogo kulinganisha na majukumu yanayomkabili mbunge.
 Dk. Kigwangalla alisema hata shida binafsi za  wananchi, wanategemea zitatuliwe na mbunge, hivyo ni vigumu mbunge kufanya kazi  bila kulipwa posho.
 “Vinginevyo wanataka mbunge arudi mitaani kuganga  njaa. Kwa hiyo, hiyo ni kauli ya unafiki, ya wanasiasa wanaotafuta umaarufu,  mimi siwezi kuiunga mkono,” alisema Dk. Kigwangalla.
 Kwa sasa mbunge analipwa Sh. 70,000 kwa siku kwa  ajili ya kujikimu pamoja na Sh. 80,000 kama posho ya kikao kwa siku ambapo jumla  analipwa Sh. 150,000 mbali na mshahara wake.
 Kwa upande wake, mbunge wa viti maalum (CCM), Dk.  Maua Daftari alipoulizwa kuhusu hoja hiyo hakuwa na jibu la kutoa.
 Badala yake mbunge huyo alibaki anaguna na kukata  simu bila ya kuiunga mkono ama kuikataa hoja hiyo.
 Akitoa maoni yake, Ali Khamis Seif mbunge wa jimbo  la Mkoani (CUF), alisema hoja ya kutaka posho ziondolewe ni nzuri lakini kwa  sasa bado sio wakati wake.
 Alisema mbunge ana kazi nyingi za kuwasaidia  wananchi hivyo ikiwa ataondolewa posho watashindwa kutatua kero mbalimbali za  wananchi.
 Hata hivyo alisema ikiwa fedha hizo zitaondolewa  kwa mbunge ziingizwe kwenye mfuko wa jimbo ili zisaidie kusukuma mbele maendeleo  ya wananchi.
 Alitoa mfano kuwa kuna wabunge wengine wanatumia  fedha hizo kuwasaidia wapiga kura wao kupata elimu pamoja na kupata matibabu  kazi ambayo ingepaswa kufanywa na serikali.
 Akizungumzia hoja hiyo, mbunge wa viti maalum  (CCM), Diana Chilolo, alisema Zitto ana mtazamo finyu juu ya hoja hiyo ya kutaka  posho ya vikao iondolewe. Alisema fedha anayoipata mbunge sio ya kwake pekee  bali inawasaidia wananchi wengine wakiwemo yatima, walemavu, wajane katika  kupata mahitaji yao.
 Kila anapokuwa mbunge wananchi wake wanamuona kama  nguzo na kimbilio lao, hivyo posho hizo zinasaidia kutatua matatizo madogo  madogo kama hayo.
 Mbunge wa jimbo la Meatu (Chadema), Meshack  Opulukwa, akitoa maoni yake alisema bado anatafakari hoja hiyo.
 Aliongeza kuwa hoja hiyo aliisikia jana, lakini  kama Waziri Kivuli wa Kilimo, Chakula na Ushirika bado anaitafakari ili kuona  kama ataiunga mkono hoja hiyo itakapopelekwa bungeni.
 Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix  Mkosamali, aliunga mkono hoja ya Zitto ya kutaka wabunge wasiwe wanalipwa posho  za vikao.
 Mkosamali alisema si posho tu, bali anataka pia  mishahara wanayolipwa wabunge pia ipungue na kuwa chini ya ile wanayolipwa hivi  sasa kwani hatua hiyo itasaidia kudhibiti mafisadi kuwania ubunge.
 “Hatuhitaji watu wagombee kwa ajili ya kupata  posho, maana kuna watu huwa wanagombea kwa lengo la kutafuta maslahi binafsi na  si kuwawakilisha Watanzania, hivyo posho ikiondolewa na mishahara ikapunguzwa  waroho wa madaraka watapungua” alisema Mkosamali.
 Aliongeza: “Kwa hiyo, naunga mkono hoja ya kufutwa  posho. Lakini mishahara ya wabunge pia ipungue, maana haiwezekani posho zipungue  wakati mishahara iko palepale,” alisema. Mkosamali alisema kufutwa kwa posho kwa  wabunge ni hatua muhimu kwani kuna maeneo mengi ya kijamii, kama vile hospitali,  fedha hizo zinaweza kupelekwa kusaidia.
 Alisema pia kupunguzwa kwa mishahara ya wabunge,  ni muhimu kwani kutasaidia kuwafanya wanaotaka kuwania ubunge, kufanya hivyo kwa  lengo la kuwawakilisha wananchi kwa dhati.
 Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David  Kafulila, naye pia aliunga mkono kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge, lakini  alishauri posho hizo zibaki kwa vikao vya watumishi wasio na mishahara, kama  vile wenyeviti wa vijiji.
 “Mtumishi yeyote alipwe posho ya vikao, ambavyo  sio sehemu ya majukumu yake,” alisema Kafulila.
 Hata hivyo, alisema malipo ya posho za vikao,  yasiishie tu kufutwa kwa wabunge, bali yafutwe serikalini na kwenye mahakama  pia.
 “Hatupaswi kulipwa kwa kukaa. Pesa nyingi inavuja.  Mfumo wa sitting allowance (posho za vikao) must end (ikomeshwe),” alisema  Kafulila.
 Alisema pia posho nyingine zote zinapaswa kutozwa  kodi na suala hilo liwe ni utaratibu na sera kwa mihimili yote ya dola; Bunge,  Serikali na Mahakama.
 Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu,  aliunga mkono si kufutwa tu kwa posho za vikao kwa wabunge, bali hata mishahara  nayo pia ifutwe akisema kazi ya ubunge haitakiwi malipo.
 “Mimi maoni yangu ni kwamba, kwa kazi ya ubunge,  wabunge hawapaswi kabisa kulipwa hata mshahara, ikifanyika hivyo itawafanya watu  kujikita zaidi katika kuwatumikia wananchi,” alisema Mangungu.
 Kwa upande wake, mbunge wa Mpanda mjini (Chadema),  Said Arf aliunga mkono hoja hiyo ya Zitto na kusema kuwa umefika wakati wabunge  kuwajali wananchi wenzao kwa kukubali kuachia posho zao ili ziweze  kuwasaidia.
 Aliwataka viongozi kupunguza anasa ili fedha hizo  zisaidie watu wenye mahitaji ya lazima ikiwemo kuwapatia maendeleo.
 Alisema mfumo unaotumiwa na Bunge wa kusema  “ndiyoooo au hapanaaa” katika kupitisha hoja mbalimbali haufai kwa kuwa huo ni  mfumo wa kijima.
 Aliongeza kuwa hoja hiyo ya kutaka posho hizo  ziondolewe inaweza kukwamishwa kwa kutumia mfumo huo wa upigaji kura kwa kusema  ndiyo au hapana.
 Juzi Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma  Kaskazini (Chadema) na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, alisema haoni sababu  mbunge kuendelea kulipwa posho nono kwa ajili ya kuhudhuria vikao kwa kuwa hiyo  ni sehemu ya kazi yao ya kila siku.
 Alisema anataka sheria ya Bunge inayotoa mwanya  kwa wabunge kulipwa posho hizo ibadilishwe haraka ili kiasi hicho cha fedha  kitumike kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania wengine wenye matatizo.
 Zitto alisema ingawa suala hilo ni gumu, lakini  ataliwasilisha katika mkutano wa Bunge la bajeti wakati atakapowasilisha bajeti  yake kama Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi.
 Alisema ana imani wabunge wenzake watakubali  pendekezo hilo na kumuunga mkono kubadilisha sheria hiyo ili posho hizo zisiwe  zinatolewa.
 Katika Bunge lililopita aliyekuwa Mbunge wa  Karatu, Dk. Willibroad Slaa (Chadema), aliwahi kutoa wazo kama hilo pamoja na  kupendekeza mshahara wa wabunge upunguzwe kwa kuwa ni mkubwa, lakini wabunge  wenzake walipinga hoja hiyo kwa nguvu zote.
 Dk. Slaa alishindwa kupitisha hoja yake katika  Bunge lililopita baada ya wenzake kukataa kumuunga mkono huku baadhi yao wakitoa  kauli za kumkejeli na kumuona kama mtu aliyekuwa akitafuta umaarufu wa kisiasa.  Kiutaratibu wabunge wote hulipwa posho ya vikao ya Sh. 80,000 kwa siku, na posho  ya kujikimu kwa kuwa nje makazi ya Sh. 70,000 hivyo kwa siku moja tu wabunge  hulipwa wastani wa Sh. 150,000 siku za kazi, wakati mwishoni mwa wiki hulipwa  Sh. 70,000, kwa maana hiyo kati ya wabunge wote waliopo ambao ni 350 kama posho  hizo zitaondolewa serikali itaokoa kiasi cha Sh. milioni 52.5 kwa siku.
 Mkutano wa Bunge la Bajeti unatarajiwa kuanza Juni  7, mwaka huu hadi Agosti 15, mwaka huu, kwa maana hiyo kutakuwa na siku za kazi  48 ambazo zitaigharimu serikali Sh. bilioni 2.52 kama posho ya vikao kwa  wabunge.
 Kiasi hicho kikiongozewa Sh. milioni 490 za posho  ya kujikimu ya mwishoni mwa wiki ambazo ni kwa siku 20, serikali itakuwa inaokoa  jumla Sh. bilioni 3.01 ambazo ni posho za wabunge bila mshahara.
 Kiasi hicho kinaweza kuelekezwa kutunisha bajeti  ya elimu, barabara au afya, ambako kuna upungufu mkubwa wa fedha.
 Mshahara wa mbunge kwa sasa ni Sh. milioni 2.5,  kiasi hicho kikichanganywa na posho ya mafuta, kuendesha ofisi mapato yake ya  ubunge yanafika kiasi cha Sh. milioni 7.19.
 Serikali inatarajia kutumia Sh. trilioni 12.8 kwa  mwaka wa fedha wa 2011/2012, kati ya hizo Sh. trilioni 8.8 ni kwa matumizi ya  kawaida, yaani posho na mishahara na ulaji mwingine, wakati fungu la maendeleo  ni Sh. trilioni nne tu.
 Utaratibu wa kupitisha bajeti ya ulaji umekuwa ni  utamaduni wa taifa hili, kwani hata mwaka huu wa fedha unaomalizika serikali  ilipitisha bajeti ya Sh. trilioni 11.6, kati yake Sh. trilioni 7.7 zilikuwa kwa  fungu la kawaida na Sh. trilioni 3.8 kwa ajili ya maendeleo.
 Soma maoni yetu ukurasa wa sita